Fri 30, Oct 2015 at 17:51:29   |  Rais akutana na waangalizi wa Uchaguzi kutoka EAC
Thu 13, Aug 2015 at 16:11:06   |  MKUTANO WA 32 WA BARAZA LA MAWAZIRI
Fri 29, May 2015 at 13:15:10   |  HOTUBA YA BAJETI MEAC 2015/2016
Mon 23, Feb 2015 at 10:29:11   |  PRESIDENT SPEECH EAC SUMMIT FEB 20, 2015
Mon 17, Nov 2014 at 16:38:03   |  EALA to Hold Plenary in Nairobi Next Week
Mon 08, Sep 2014 at 11:36:07   |  House Passes Key Resolution on PWDs

KAMATI YA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAMALIZA ZOEZI LA UKUSANYAJI WA MAONI TANZANIA.

 

Ikiwa ni moja kati ya hatua muhimu inayolenga kuiimarisha na kuitangaza sekta binafsi, Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia kamati ya Kilimo, Maliasili na Utalii ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Jana, Tarehe 17 Septemba, 2014 iliendesha zoezi la ukusanyaji maoni lililofanyika kwenye Hoteli ya Tiffany Diamond Jijini Dar-es-Salaam, kutoka kwa wadau wa makundi mbalimbali  ya sekta binafsi za Tanzania. Maoni yaliyotolewa na wadau hao yatatumika katika kurekebisha na kuimarisha mswaada wa Sheria ya vyama vya Ushirika ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Awali zoezi hili la ukusanyaji maoni lilifanyika katika Nchi wanachama zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki za Kenya, Rwanda, na Burundi kabla ya kufanyika hapa Tanzania Jana Tarehe 17 Septemba, 2014.

 

Tanzania imeshiriki katika zoezi hili muhimu ikiwa na Jumla ya Idadi ya vyama  vya Ushirika 9,964 vilivyo sajiliwa kisheria, vikiwa na Jumla ya wanachama zaidi ya Milioni mbili na laki tano (2500000.)

 

Akifungua zoezi hilo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za uzalishaji Dkt. Abdullah Makame kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Ushirikiano  wa Afrika Mashariki alisema  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatoa maoni kwa maandishi juu ya musuada wa Sheria hiyo.

 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mjumbe wa Kamati  hiyo ya Kilimo, Maliasili na utalii Mh. Mike Ssebalu kutoka Uganda alisema  vyama vya Ushirika ni chombo muhimu cha kupitisha taarifa za fursa za masoko na mitaji kwa wakulima wadogo wadogo na watoa huduma katika Nchi Wanachama.

 

Kamati ya Kilimo, Maliasili, na Utalii ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na Wajumbe kumi na tano (15) ikijumuisha wajumbe watatu kutoka kila Nchi Mwanachama.

 

Mh. Mike Ssebalu aliongeza kusema “Tukizikuza na kuzijengea uwezo Sekta binafsi zitaongeza fursa za ajira kwa vijana na kuongeza kasi ya ushiriki wa sekta hizo katika kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki”.

 

Aidha Mwenyekiti wa Mtandao wa Wakulima wa Afrika Mashariki Ndug. Philipo Kihiro akitoa mchango wake wakati wa zoezi hilo  alisema “ilikuwa ni muhimu kwa chombo hiki kushirikisha  vyama vyetu  vya Ushirika katika kuwaweka pamoja na kuimarisha umoja  wa  wakulima wadogo wadogo ili kuwawezesha kufanya kilimo Biashara”.

 

Umuhimu wa Mswaada wa Sheria hii ya Vyama vya Ushirika ya Afrika Mashariki pamoja  na mambo mengine itawawezesha wakulima wadogo wadogo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kujipatia fursa za masoko, kubadilishana uzoefu wa Kilimo na Teknologia hivyo kuwaongezea uzalishaji na kipato kitakacho boresha maisha yao.

 

Baada ya kumaliza zoezi hilo hapa Nchini Tanzania Jana Tarehe 17Septemba, 2014 tume hiyo ya ukusanyaji maoni ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki leo, Tarehe 18 Septemba, 2014 itahitimisha mchakato huo  Nchini ya Uganda.  

 

Na Teodos Komba