Fri 30, Oct 2015 at 17:51:29   |  Rais akutana na waangalizi wa Uchaguzi kutoka EAC
Thu 13, Aug 2015 at 16:11:06   |  MKUTANO WA 32 WA BARAZA LA MAWAZIRI
Fri 29, May 2015 at 13:15:10   |  HOTUBA YA BAJETI MEAC 2015/2016
Mon 23, Feb 2015 at 10:29:11   |  PRESIDENT SPEECH EAC SUMMIT FEB 20, 2015
Mon 17, Nov 2014 at 16:38:03   |  EALA to Hold Plenary in Nairobi Next Week
Mon 08, Sep 2014 at 11:36:07   |  House Passes Key Resolution on PWDs

WAZIRI MWAKYEMBE AKAMILISHA ZIARA YA WILAYA YA TARIME

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (MB), amefanya ziara ya siku mbili ya kutembelea Wilaya ya Tarime katika Mkoa wa Mara ili kuhamasisha wananchi kutumia fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, ziara hiyo ililenga kuhamasisha wananchi kutambua kwamba pamoja na ushirikiano wa kindungu uliopo baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia kuna ushindani wa kibiashara ambao Watanzania inabidi washiriki.

Waziri Mwakyembe aliwasili Musoma Mei 8 na kufanya kikao na Uongozi wa Mkoa wa Mara. Mei 9 alianza kwa kukutana na viongozi wa Wilaya ya Tarime na kuwaeleza umuhimu wa viongozi hao kusimamia sheria na kuhakiisha wanawasaidia wakulima na wafanyabiashara waweze kutumia fursa zilizopo kwenye soko la Afrika Mashariki.

Baadae Waziri alitembelea Mpaka wa Sirali ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa Vituo vya Utoaji Huduma za Mipakani kwa Pamoja (One Stop Border Posts) vya Sirali (Tanzania) na Isbania (Kenya).

Waziri Mwakyembe alianza ukaguzi kwa kutembelea upande wa Kenya ambapo aliridhishwa na ubora wa jengo hilo lakini alisikitishwa na jengo la upande wa Tanzania kutokana na  kujengwa chini ya kiwango.

Waziri aliahidi kuchukua hatua kwa wahusika wote walioshiriki kusababisha jengo hilo kuwa chini ya kiwango. Jengo hilo lilionekana kuwa na nyufa, na vifaa vilivyotumika kujengea kuonekana kuanza kuharibika hata kabla jengo hilo kuanza kutumika. 

Baadae mchana Waziri alikutana na Wakulima na Wafanyabiashara wa Wilaya ya Tarime ambao husafirisha bidhaa zao za mazao na mifugo katika Nchi jirani ya Kenya.

Waziri alisikiliza kero za wakulima na Wafanyabiashara ambapo wengi walilalamikia vikwazo vingi wanavyovipata wakati wa kusafirisha bidhaa zao, kutozwa ushuru mara mbili yaani ushuru wa mazao na wa soko.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri alikemea Wafanyakazi wa umma wasiokua waaminifu kwa kujihusidha na vitendo visivyotakiwa kama vile rushwa wanapotoa huduma zao mipakani. Aliwataka wawe wazalendo na wajiepushe kuwa ni watu ambao wanakua kikwazo kwa wafanyabiashara.

Pia aliwataka wafanyakazi hao wasimamie sheria ili wakulima wasinyonywe kupitia mtindo wa lumbesa ambapo magunia ya mazao hujazwa kupita kipimo kinachotakiwa cha kilo 100.

Waziri alitangaza rasmi vita dhidi ya lumbesa nchini kote na kusema kuwa sheria ikisimamiwa hakuna mtu atafanya biashara ya lumbesa. Sheria ya Uzito na Vipimo inatoa adhabu ya faini ya Sh. 10,000 au jela miaka mitatu au vyote.

Waziri aliahidi kuwa Wizara itazunguka Nchi nzima kwenye Mikoa ya mipakani ili kutoa elimu kwa Watanzania waweze kutumia fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Fursa katika Mpango wa Afrika na Marekani yaani AGOA. Mchango wa Tanzania AGOA umeshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2000 hadi asilimia 4 mwaka huu lakini mchango wa Kenya umekua kutoka asilimia 56 mwaka 2000 hadi asilimia 96 mwaka huu.

Ends